22 Septemba 2019 - 06:18
Watu 18 wauawa katika mapigano baina ya vikosi vya Haftar na serikali, Libya

Kwa akali watu 18 wameuawa katika makabiliano makali baina ya vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya vinavyoongozwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar na vile vya serikali ya mwafaka wa kitaifa kusini mwa mji mkuu, Tripoli.

(ABNA24.com) Kwa akali watu 18 wameuawa katika makabiliano makali baina ya vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya vinavyoongozwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar na vile vya serikali ya mwafaka wa kitaifa kusini mwa mji mkuu, Tripoli.

Duru za kijeshi zinasema askari 11 wa serikali inayotambuliwa na jamii ya kimataifa wameuawa katika mapigano hayo ya jana Jumamosi.

Wakati huohuo, Ahmad al-Mismari, msemaji wa vikosi vya kamanda muasi Khalifa Haftar amesema wapiganaji saba wa genge hilo wameuawa katika mapigano hayo, yaliyotokea karibu na makutano ya barabara ya kuelekea uwanja wa ndege, yaani barabara za Salah al-Din na Ain Zara (kusini mwa Tripoli), na kwamba makumi ya wengine wamejeruhiwa.

Haya yanajiri siku chache baada ya askari 14 wa vikosi vya serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya kuuliwa katika mashambulio ya anga yaliyofanywa na vikosi vya Haftar vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi, huko kusini mwa mji mkuu huo.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, karibu watu elfu moja wameuawa, zaidi ya elfu tano wamejeruhiwa na wengine zaidi ya laki moja wamelazimika kuhama nyumba na makazi yao, tangu vikosi vya Khalifa Haftar vilipoanzisha mashambulio dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli tarehe 4 Aprili mwaka huu.

Kwa mwaka wa nane sasa nchi hiyo imekuwa na tawala mbili, mmoja ukiwa ni wa bunge lenye makao yake katika mji wa mashariki wa Tobruk likiungwa mkono na vikosi vya jeshi la taifa la Libya vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na utawala mwengine wa serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, ambayo makao yake yako mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.



/129